Kagame kiburi
September 1,
2013,
*Wanaompa jeuri
sasa waanikwa, yamo mataifa makubwa
*Vyombo vya
kimataifa vyatumika kumkingia kifua kila kona
*Uamuzi wa
Kenya, Uganda, kujitoa bandari Dar wahusishwa
Na Mwandishi
Wetu
RAIS wa Rwanda
Paul Kagame bado anaonekana kuwa na kinyongo na Rais Jakaya Kikwete tangu
alipopewa ushauri wa kukaa meza moja na waasi ili kumaliza migogoro iliyopo.
Hata hivyo
imeelezwa kuwa Rais Kagame anaonekana kuwa na kundi nyuma yake ambalo linampa
kiburi na kujiamini kwa kila anachokifanya na ndio maana hakuna mahali ambapo
anaonesha kuwa tayari kutumia busara kumaliza tofauti iliyojitokeza.
Tayari Rais
Kikwete ameweka wazi kuwa Serikali yake haipo tayari kuingia kwenye malumbano
na Rwanda wala nchi nyingine yoyote na kwamba kuhusu Rwanda busara itatumika
kutafuta ufumbuzi wake.
Kauli ya Rais
Kikwete imekuja baada ya Rais Kagame kutoa kauli za kejeli baada ya kushauriwa
na Rais Kikwete kuwa ni vema akakaa na vikundi vya waasi kutafuta ufumbuzi wa
kumaliza migogoro nchini Rwanda, ushauri ambao unaonesha kutomfurahisha Kagame.
Wakizungumza
wiki hii baadhi ya wachambuzi wa siasa za kimataifa, wameliambia Jambo Leo
Jumapili kuwa Rais Kagame anaonekana kuwa na kiburi na hiyo inatokana na
kutumia mataifa mengine kuonesha kukasirishwa kwake na ushauri wa Rais Kikwete.
Kwa mujibu wa
wachambuzi hao, ni kwamba Rais Kagame anapata kiburi kwasababu pia kuna mataifa
makubwa ambayo yanampa msukumo wa kutaka uhusiano wa nchi hizo mbili kuendelea
kuwa kwenye kutetereka ingawa Serikali ya Tanzania imezidi kuweka wazi
uhuasiano wa nchi hizo si mbaya kama ambavyo inaelezwa.
Kitendo cha
Rais wa Rwanda Paul Kagame kutokuwa tayari kuumaliza mgogoro huo, mjadala
mkubwa umezidi kuibuka kutokana na kutetereka kwa uhusiano kati ya Tanzania na
Rwanda huku Rais wa Paul Kagame akidaiwa kuwa ana kiburi ndio maana hadi sasa
hajaonesha kutokuwa tayari kukaa kwenye mazungumo kutafuta muafaka
Wakizungumzia
zaidi nguvu ya Rais Kagame, ni kwamba inawezekana pia inatokana na namna
ambavyo anatumia vyombo vya habari vya kimataifa kuelezea uhusiano wake na
Tanzania.
Pia nguvu ya
wanaomuunga mkono Rais Kagame imedaiwa kuwa ndio inayoendelea kumpa kiburi cha
kutokuwa tayari kukaa na vikundi vya waasi kutafuta suluhu.
Wakati hayo
yakiendelea duru za kimataifa zinafafanua kuwa Rais Kagame huenda anapata
kiburi kutokana na kupewa nguvu na aliyewahi kuwa Rais wa Marekani Bill
Clinton.
Siku za hivi
karibuni baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa na mitandao ya kijamii
vimemnukuu Clinton akitoa kauli za kumkingia kifua Rais Kagame.
Rais Kagame
amekuwa akituhumiwa kufadhili kundi la waasi la M23 ambalo lipo kwenye mapigano
ya muda mrefu nchini Congo lakini pia Clinton alinukuliwa akimtetea Rais Kagame
na kumsafisha dhidi ya tuhuma hizo.
Hata hivyo Rais
Kagame mwenyewe amekuwa akikanusha kuhusika kulifadhili kundi hilo kwa namna
yoyote ile, na hilo amekuwa alisisitiza mara kwa mara inapotokea mataifa mengi
kumtuhumu.
Taarifa zaidi
kuhusu Rais Kagame, kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya
kimataifa, vinadai kuwa mbali ya Clinton kumtetea pia baadhi ya nchi za
Jumuia ya Afrika Mashariki nazo zinaonekana kumuunga mkono harakati zake za
kuiendelea kutokuwa na uhusiano mzuri na Tanzania.
Miongoni mwa
wanaotajwa kuwa nyuma ya Rais Kagame ni baadhi ya viongozi wa Serikali ya
Uganda na hiyo inatokana na kile kinachoelezwa kuwa aliwahi kuwa Mkuu wa
Idara ya Usalama wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda kabla ya kujiunga na chama
cha RPF.
Ushirika huo wa
Kagame kwa Rais Museveni, unatajwa kuwa ndicho kinachotafsiriwa sasa kwamba
kinawafanya waendelee kushirikiana.
Pia
ilibainishwa kwamba ushirika wa Marekani chini Clinton kwa Kagame, ulikuwa
umeshika kasi na hivyo kufanya Taifa hilo kubwa Duniani kukiunga mkono chama
cha RPF alimokuwa Kagame.
Kwa mujibu wa
taarifa zilizosambaa katika baadhi ya mitandao ya kijamii, jeuri hiyo ya kuwa
na vigogo wanaomkingia kifua, ndio inayompa uwezo Kagame kuendelea kuvuruga
uhusiano baina ya nchi yake na baadhi ya nchi nyingine ikiwemo Tanzania.
Taarifa zaidi
zilidai kuwa hata kitendo cha Rwanda kuamua kujitoa kutumia Bandari ya Dar es
Salaan kupitisha mizigo yao ikiwa ni sehemu ya kuonesha hasira zake dhidi ya
Tanzania.
Mbali ya Rwanda
pia Uganda na Kenya nazo zimejiondoa kutumia bandari hiyo na sasa wamepanga
kutumia bandari ya Mombasa.
Kabla ya uamuzi
huo wa kujiondoa nchi za Uganda na Rwanda zilikuwa zikitumia bandari ya Dar es
Salaam kama kituo cha kupitishia mizigo yao.
Uamuzi wa
kutotumia bandari ya Dar es Salaam kwa nchi hizo unaanza leo (Septemba Mosi),
unafanyika baada ya mazungumzo ya faragha yaliyomshirikisha Rais Kagame na Rais
Museveni na Serikali ya Kenya.
Wakati hayo
yakiendelea, Watanzania na Afrika Mashariki imeshuhudia pia wabunge wa Jumuia
ya Afrika Mashariki (EALA), wakishindwa kufanya kikao cha Bunge hilo baada ya
kutolewa hoja kuwa umefika wakati kwa wabunge wa Bunge hilo kufanya mikutano
yao kwa kuzunguka nchi husika.
Hoja hiyo
inaonekana ni mwendelezo wa kulipa kisasi dhidi ya Tanzania kwani ukiondoa
wabunge wanaowakilisha nchi hii, wabunge kutoka Rwanda, Kenya, Uganda na
Burundi wameamua kuunga mkono licha ya kwamba haikuwa sehemu ya ajenda ambayo
itajadiliwa kwenye kikao hicho.
Akizungumza
kwenye kikao hicho hivi karibuni, Mbunge kutoka nchini Kenya Peter Mathula,
aliamua kuwasilisha hoja binafsi akitaka kutenguliwa kwa uamuzi wa vikao vya
Bunge hilo kufanyika tu mjini Arusha Tanzania.
Vikao hivyo
vimekuwa vikifanyika Arusha nchini Tanzania ambako ndiko makao makuu ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Mbunge huyo alijenga ushawishi kwa wabunge wa Bunge hilo,
kukubali vikao hivyo kufanyika kwa mzunguko katika maeneo ya nchi hizo
zinazounda Jumuia hiyo.
Hata hivyo
kuwasilishwa kwa hoja hizo, kulizua malumbano huku wabunge wa Tanzania
wakionekana pekee wakiipinga hoja hiyo.
Mbunge wa EALA
kwa upande wa Tanzania Abdullah Mwinyi, aliongoza wabunge wa Tanzania kutoa nje
ya ukumbi wa Bunge na kususia kikao hicho.
Hatua ya
wabunge wa nchi zote zinazounda Bunge hilo kuwa na umoja wa kupinga vikao hivyo
kufanyika Tanzania, imetafsiriwa kuwa ni mwendelezo wa mpango wa kuvuruga umoja
uliokuwapo hapo awali.
Hata hivyo,
baada ya mvutano huo, kikao cha uongozi wa Bunge hilo, kilifikia makubaliano ya
vikao hivyo kufanyika kwa mzunguko.
Bunge la
Tanzania kutokana na uhusiano tete kati ya Tanzania na Rwanda, wiki hii
limeamua kuomba msimamo wa Serikali ya Tanzania ili kujua namna ambavyo
limejipanga kutafuta suluhu.
Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe aliitaka Serikali kuelezea msimamo wake
hasa kutokana na kuonekana Rais Kagame hakufurahishwa na ushauri wa Rais
Kikwete ambapo Waziri Mkuu Pinda wakati anatoa msimamo alisema Serikali ya
Tanzania inaamini busara itatumika kupata ufumbuzi wake.
Pinda alisema
Rais Kikwete ameeleza kwa kina kuhusu chanzo cha kutokuwepo kwa uhusiano mzuri
na Rwanda , lakini bado alifafanua kuwa tayari Rais Kikwete amemuomba Rais
Museveni kusaidia kupata kwa ufumbuzi wa suala hilo.
“Serikali
tuaamini kuwa tutamaliza suala hilo kwa kutumia busara zaidi.Tunatambua heshima
yetu kwa nchi za Afrika Mashariki na kubwa zaidi tumekuwa wasuluhishi wazuri wa
migogoro kwenye nchi za Afrika Mashariki.Hivyo busara itatumika kupata
suluhu,”alisema Pinda na kuongeza “Serikali hatutapuuza haya yanayoendelea,”.
Mbowe katika
maelezo yake bungeni alisema ana hofu na ushirikiano uliopo hasa baada ya
Tanzania imeanza kutengwa na baadhi ya nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki.
Alisema hatua
ya nchi za Rwanda, Kenya na Uganda kuendesha vikao kupitia wakuu wa nchi
ikiwemo kujitoa kwa nchi ya Rwanda kutumia Bandari ya Dar es Salaam,
kunaashiria mwelekeo mbaya.
Rais Museveni
ndiye Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika Mashariki, na ndio maana ameombwa na
Tanzania kuwa msuluhishi wa mgogoro kati ya Tanzania na Rwanda,
unaoendelea chini kwa chini kati ya nchi mbili hizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni